Wajumbe wa ALAT tawi la mkoa wa Katavi wamepongeza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda kwa kuwa na mradi wa maji mkubwa na unaotumia umeme jua. Pongezi hizo zimetolewa na mwenyekiti wa ALAT wa mkoa wa Katavi Mstahiki Meya William Mbogo.
“Nawapongeza watalaam pamoja na ofisi ya Mkurugenzi kwa kuwa na mradi unaotumia umeme jua. Halmashauri zingine tujifunze kuwa na miradi ya maji inayotumia umeme jua kama wenzetu wa Mpanda DC walivyofanya….”
Mradi wa maji ya bomba katika kijiji cha Majalila umegharimu shilingi 703,501,240 hadi kukamilika kwake. Mradi umetekelezwa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza ilikuwa ujenzi wa matenki mawili yenye ujazo wa lita 180,000 na ufungaji mabomba ya maji ‘civil works and pipe fitting’. Hata hivyo awamu ya pili ilijikita katika ufungaji wa umeme jua, utengenezaji wa ua na pampu ya kuvuta maji.
Wakazi wa kijiji cha Majalila ambapo ndipo panapojengwa makao Makuu ya halmashauri ya wilaya ya Mpanda wananufaika na mradi huo kwa kupata maji safi na salama.
Hata hivyo, kamati ya ALAT tawi la Katavi iliendelea na ukaguzi wa miradi iliyopitiwa na mwenge wa Uhuru 2017 katika halmashauri ya wilaya ya Mpanda. Miradi hiyo ni pamoja na jengo la utawala la shule ya sekondari Mpandandogo uliogharimu shilingi 64,680,396.40.
Miradi mingine ni vyumba sita vya madarasa na ofisi moja katika shule ya msingi Kasekese. Halmashauri ya wilaya ya Mpanda imeshirikiana bega kwa bega na wananchi wa Kasekese kuhakikisha kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa.
“Mheshimiwa mwenyekiti, shule ya msingi Kasekese ina zaidi ya wanafunzi 1,600 na robo tatu yao walikuwa wanasomea nje. Kukamilika kwa ujenzi wa vyumba sita vimesaidia sana kuongeza hamasa ya wanafunzi ya kupenda shule….” Alisema Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw.Romuli John.
Hata hivyo kamati ya ALAT iliendelea na ukaguzi wa mradi wa zahanati ya kijiji cha Itetemya unaotekelezwa kwa ufadhili wa serikali kuu kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF III kwa kushirikiana halmashauri ya wilaya ya Mpanda pamoja na wananchi wa kijiji hicho. Mradi huo umegharimu shilingi 76,391,800. Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya kuishi walimu sita, vyumba vitatu vya madarasa na matundu matano ya vyoo vilivyojengwa katika shule ya sekondari ya Ikola.
Baada ya wajumbe kutembelea miradi iliyopitiwa na mwenge, walihitimisha kwa kufanya kikao cha majumlisho. Kikao hicho kilifanyikia katika ukumbi wa mwolo wa Ikola katika kijiji cha Ikola. Kikao kilimuidhinisha Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw. Romuli Rojas John kuwa katibu wa ALAT tawi la Katavi kushika nafasi ya aliyekuwa katibu wa ALAT Bw. Ngalinda Ahmada aliyefariki Dunia Disemba 01, 2016.
Wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuwa fundi wa kawaidi (local fundi) anapojenga mradi katika halmashauri zilizopo mkoani Katavi asilipwe fedha nyingi. Inatakiwa alipwe kutokana na kazi aliyofanya na siyo kumpatia hela nyingi ambazo haziendani na alichofanya katika mradi. Mafundi wengi wamekuwa wanachelewesha kazi kwa kuwa wao ndio wanaodaiwa kukamilisha kazi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.