Karema.Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda limepongeza walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Karema kwa kupata matokeo mazuri ya mtihani wa kidato cha sita 2017. Wanafunzi hao wa shule ya sekondari Karema wameongoza kwa mkoa wa Katavi kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya shule tatu na nafasi ya 50 kitaifa kati ya shule 449.
Pongezi hizo zimetolewa na diwani wa kata ya Karema mhe. Michael Kapata wakati wa mkutano wa baraza Julai 25, 2017 uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda(Idara ya maji).
“Mhe. Mwenyekiti shule ya Karema imetuweka katika ramani ya Tanzania. Mpaka sasa tunazidi kupokea wanafunzi waliopangiwa kuja kuanza kidato cha tano kwa wingi kutokana na matokeo mazuri tangu kuanzishwa kwa kidato cha tano na sita. Ni muda mwafaka wa Halmashauri kuwapongeza walimu na bodi ya shule ya Karema kama njia ya kuwashukuru”. Alisema mhe. Kapata.
Mhe. Kapata amekuwa msitari wa mbele kwa kuisemea shule hiyo ya sekondari ya Karema katika vikao vya waheshimiwa madiwani na kufuatilia maendeleo yake kwa karibu. Wanafunzi waliomaliza kidato cha sita katika sekondari ya Karema mwaka 2017 walikuwa 74 na wanafunzi 15 wamepata daraaja la kwanza( Division I), wanafunzi 50 daraja la pili (Divisioni II) na wanafunzi 9 wamepata daraja la tatu (Division II).
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Mhe. Hamad Mapengo ameahidi kuendelea kumkumbusha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda kuhakikisha anatekeleza ahadi zilizoahidiwa kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka 2016. Wanafunzi hao walimwahidi mgeni rasmi kuwa watafanya vizuri katika mtihani wa kuhitimu kidato cha sita.
“Nikwambie tu Mkurugenzi, mwaka huu 2017 kama uongozi wa shule ungenialika kuwa mgeni rasmi katika shule ya sekondari Karema nisingekubali. Mwaka jana Halmashauri iliahidi kuwa kila mwanafunzi wa kidato cha sita atakayepata daraja la kwanza atapewa shilingi 50,000, daraja la pili 40,000 na daraja la tatu 30,000. Katika ahadi zilizotolewa, aliyetekeleza ni Mbunge wa Mpanda vijijini Mhe. Moshi Kakoso”. Alisema Mhe. Mapengo
Kwa matokeo ya kidato cha sita mwaka 2016, Karema ilikuwa nafasi ya 61 Kitaifa kati ya shule 423 na ya kwanza kwa mkoa wa Katavi kati ya shule 3. Wanafunzi 10 walipata daraja la kwanza, 46 daraja la pili na daraja la tatu wanafunzi 10.
Hata hivyo Mbunge wa jimbo la Mpanda vijijini Mhe. Kakoso aliwaasa madiwani kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Wanafunzi wanaofanya vizuri katika shule ya sekondari Karema katika matokeo ya kidato cha sita, asilimia kubwa wanatoka nje ya mkoa wa Katavi. Ni wajibu wa waheshimiwa madiwani kushirikiana na watalaam wa Halmashauri kuona namna ya wanafunzi wa ngazi ya chini nao wafanye vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha 4 na wao wapate nafasi za kujiunga kidato cha 5 na 6.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.