Halmashauri ya wilaya ya Mpanda imerasmisha eneo la uwekezaji la Luhafwe na kupanga sehemu ya eneo kuwa mji wa biashara. Hayo yamesemwa Juni 22, 2017 na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw. Salehe Mhando kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wanaoishi eneo hilo la Luhafwe.
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Mhando aliongozana na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Mhe. Hamad Mapengo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw.Romuli John akiwa na watalaam wake.
Kabla ya kuanza mkutano, Afisa Mipango miji Bw. Elisha Mengele aliwapitisha wajumbe na viongozi wa eneo hilo na kuwaonesha mipaka ya eneo la makazi.
Eneo hilo la makazi lina ukubwa wa Hekta 2400 na tayari michoro mitatu yenye viwanja vya makazi 2164 imekamilika. Viwanja hivyo vitakuwa vya makazi tu na ukubwa umezingatia vipimo vya mjini na siyo mashamba.Pia huduma za kijamii nazo zimezingatiwa na kutengwa. Mfano shule, zahanati, maeneo ya wazi na huduma zingine za kibinadamu.
Aidha, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw.Mhando amewaagiza wale wote wanaoishi katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kilimo, Ufugaji au utalii wasitishe shughuli zao na kusubiria utaratibu watakaopangiwa na wataalam wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Mhe. Hamad Mapengo aliwashauri wakazi wa Luhafwe kukubaliana na utaratibu wa wataalam wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda.
“Huu ni mji na siyo kijiji wala kitongoji, tunahitaji kupaendesha kimji na kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi”. Alisema Mhe. Mapengo
Hata hivyo, Mhe. Mapengo aliwashauri wakazi wa Luhafwe wasiishi kwa mazoea kama zamani walipokuwa wanavamia maeneo na kujimilikisha mashamba makubwa bila utaratibu. Sasa utaratibu utaanza kufuatwa na wale watakao kiuka masharti na utaratibu, wakiondolewa kwa nguvu wasilalamikie viongozi.
Mpango wa matumizi wa Ardhi ya eneo la Uwekezaji (Luhafwe) umetekelezwa kwa mujibu wa sheria Na. 6 ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2007, sheria ya Mipango miji Na. 8 ya mwaka 2007, sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999, sheria ya usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004, sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 na sheria ya maji Na. 1 ya mwaka 1999.
Lengo kuu la sheria hizi ni kuhifadhi Ardhi na Mazingira na kuyatumia katika namna ambayo ni endelevu kwa Matumizi ya vizazi vya sasa na vijavyo, kuongeza thamani ya Ardhi na tija katika uzalishaji mali na kuwa na Ardhi iliyopangiliwa katika utaratibu maalumu na kugawa kwa watu na wawekezaji kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria.
Maeneo yaliyotengwa katika eneo la uwekezaji( Luhafwe) ni eneo la makazi lenye ukubwa wa Hekta 2400, eneo la viwanda Hekta 730, Utalii Ikolojia eneo la ukubwa wa Hekta 5036.Maeneo mengine yaliyotengwa ni eneo la kilimo wenyeji Hekta 4372, Kilimo uwekezaji Hekta 11,000 na malisho wenyeji Hekta 2000.
Hata hivyo kuna eneo lililotengwa kwa malisho ya mifugo uwekezaji Hekta 11,000 na benki ya ardhi Hekta 4,164.
Maeneo mengine ni uwekezaji wa jeshi la SUMA-JKT Hekta 3,000 na JKT kambi Hekta 1,000 na eneo lililiobakia la ukubwa wa hekta 1,298 ni msitu wa hifadhi. Eneo lote la uwekezaji la Luhafwe lina jumla ya ukubwa wa Hekta 46,000.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.