Madiwani Wilayani Tanganyika wametakiwa kuwa mabalozi wa kwanza kuhamasisha Kilimo cha zao la Pamba kwa vitendo Mkoani humo ili kuleta hamasa kwa Wananchi kulima zao hilo na hivyo kuondokana na umasikini.
Rai hiyo imetolewa na Balozi wa zao la Pamba Nchini na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw.Agrey Mwanri katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika katika kikao cha tathmini ya Ziara yake aliyoifanya Wilayani humo iliyolenga kuhamasisha Wananchi kushiriki katika kilimo cha zao la Pamba.
Balozi Mwanri amewaambia Madiwani Wilayani Tanganyika kuwa endapo kila diwani ataamua kulima ekari moja ya Pamba katika eneo lake kwa kuzingatia kanuni na mbinu za kisasa za kilimo cha zao hilo, itatoa Hamasa kubwa kwa Wananchi kushiriki katika Kilimo cha zao la Pamba jambo litaloleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika Wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi kwa ujumla.
“Tusaidieni,kampeni ya kwenu inapenya kuliko kampeni ya Balozi kwa sababu nyinyi ni viongozi na mnabeba zamana,na endapo hamtawajibika na kuhamasisha nyinyi mtakua wa kwanza kuwajibika”alisema Balozi huyo wa zao la Pamba Agrey Mwanri.
Amesema ni muhimu uongozi kuhamasisha Wananchi kuzalisha mazao mbalimbali kwa ziada ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo Wilayani Tanganyika na Mkoa wa Katavi kwa ujumla.
Aidha Balozi Mwanri ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa Kampeni ya hamasa ya zao la Pamba inafanikiwa kwa sehemu kubwa.
Awali akitoa taarifa ya tathmini ya Kampeni ya zao la Pamba iliyofanyika Wilayani Tanganyika Afisa Kilimo,Mifugo na Ushirika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw.amesema Vijiji 10 katika Hamashauri ya Wilaya ya Tanganyika vimefikiwa na Elimu ya kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la Pamba.
Amevitaja vijiji vilivyofikiwa na Kampeni hiyo kuwa ni Katobo,Kayenze,Bulamata,KabageKabatini,Mpembe,Kamsanga ,Mpembe,Mnyagala,ambapo zaidi ya wakulima wa zao la Pamba 1014 wamefikiwa na Kampeni hiyo yenye lengo la kuhamasisha mbinu bora na za kisasa za Kilimo cha zao la Pamba.
Kwa Upande wao madiwani wa Hamashauri ya Wilaya ya Tanganyika wameahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha zao la Pamba kwa vitendo ambapo wameahidi kulima zao la Pamba kisasa ili kutoa hamasa kwa Wananchi kulima zao hilo.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.