Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw. Salehe Mhando ameahidi kuimarisha ulinzi kwa wanafunzi na watoto wote kwa ujumla. Mhando ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kwa mkoa wa Katavi yamefanyikia Mishamo katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda. Wajibu wa wazazi ni kuhakikisha mtoto anatimiziwa mahitaji muhimu lakini suala la ulinzi ni la wazazi na serikali.
“Viongozi na watendaji wa serikali tuchukue hatua kwa wanaopuuzia suala la haki za watoto. Watoto wanalindwa kwa sheria ya mwaka 2009”. Alisema Mhando
Mke wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne mama Salma Kikwete alisema, “mtoto wa mwenzio ni mwanao”. Jamii ichukulie kuwa ina wajibu wa kuwalinda watoto wote kwa haki na usawa katika maeneo wanayoishi. Wazazi na walezi wameshauriwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola pindi wanapoona watoto wakitendewa vitendo visivyo vizuri.
Watu wengine wamefikia hatua ya kuwa na roho ya ukatili, mpaka wengine wanawabaka watoto wadogo na kuwasababishia maumivu na wengine kufariki Dunia. Wanaume wengine wanaoa watoto kwa kuwarubuni na kuwakatisha masomo. Sasa atakayesubutu kumpa mimba mwanafunzi ataenda jela miaka 30. Alisema Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw. Mhando
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw.Romuli John amewashauri wazazi na walimu washirikiane kubaini wanafunzi wanaotoka maeneo hatarishi ili waone namna ya kuwaimarishia ulinzi. Watoto walio chini ya miaka 10 wasiachwe peke yao kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 6 tena unakuta wanaishi mashambani.
Badala yake wanapaswa wale wanafunzi wenye umri mkubwa ndio waongozane na watoto wadogo. Watoto ambao wanatoka sehemu ambazo hazina wanafunzi wakubwa itabidi wazazi wawe wanawasindikiza watoto hao hadi shuleni na baadaye kuwafuata baada ya masomo.
Maeneo mengi katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda, nyumba ziko mbali sana na shule. Sasa ni vigumu mwanafunzi kurudi nyumbani kula chakula cha mchana na arudi tena shuleni kusoma ili kukamilisha ratiba ya masomo ya siku. Ndiyo maana uongozi wa shule na serikali waliwaagiza wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi ili wawe wanakula shuleni.
Mtoto hawezi kufanya vizuri kimasomo kama muda mwingi anakuwa na njaa na bado akirudi nyumbani anakuwa hana uhakika na kupata chakula. Kibaya zaidi unakuta mtoto anakaa na watoto wenzake nyumbani huku wazazi wakiwa mashambani au kwenye shughuli za kibiashara.
Bw.John alikabidhi mipira ya miguu kwa shule 6 na mpira mmoja kwa Mtendaji wa kata ya Mishamo kwa lengo la kuhimiza mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Tanzania na nchi nyingine barani Afrika zinaungana kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Juni 16 kama ilivyoazimiwa na nchi wanachama 51 wa Umoja wa Afrika mnamo mwaka 1990.
Ikiwa siku hii ni siku kubwa barani Afrika, hivyo kila nchi mwanachama anatakiwa kuiadhimisha kulingana na makubaliano, hivyo kitaifa siku hii inaadhimishwa mkoani Dodoma ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi Na Fursa Sawa Kwa Watoto.”
Ikumbukwe kuwa azimio hili lilipitishwa rami mwaka 1990 maalum kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto, Afrika ya Kusini Juni 16, 1976 pale utawala wa Makaburu ulipowaua kikatili watoto waliokuwa wakidai haki ya kutokubaguliwa kutokana na rangi yao ambayo ni haki yao kimsingi wa haki za binadamu.
Ama kwa hakika kaulimbiu ya mtoto wa Afrika ya mwaka huu imelenga kusisitiza juu ya uzingatiaji wa jukumu la ulinzi wa mtoto na utoaji wa haki sawa kwa watoto wote ili kufikia malengo endelevu ifikapo mwaka 2030.
Siku ya maadhimisho ya mtoto wa Afrika ni mahsusi kwa taifa na jamii kwa ujumla kutafuta changamoto, vikwazo na matatizo yanayomkabiri mtoto katika nyanja zote muhimu kama malezi, malazi, makazi, haki zake za msingi katika jamii na si tu kuadhimisha kama sherehe bali uwe ni uwanja wa kutatua shida zinazomkumba mtoto.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.